Utafiti huu ulilenga kuchunguza makosa ya kimatamshi yanayofanywa na wanafunzi wa shule za upili za umma katika Tarafa ya Rigoma, Kaunti ya Nyamira, Kenya. Lengo kuu lilikuwa kuelewa aina za makosa ya kimatamshi, vyanzo vyake, na mikakati ya kurekebisha makosa hayo ili kuboresha ufasaha wa matumizi ya Kiswahili sanifu miongoni mwa wanafunzi. Utafiti huu ulitumia mbinu mchanganyiko za uchunguzi ikiwemo kujaza hojaji, mahojiano na walimu na wanafunzi. Uchambuzi wa data ulifanywa kwa kwa kutumia takwimu na maelezo ya kina.Matokeo yalionyesha kuwa makosa ya kimatamshi yanasababishwa zaidi na ushawishi wa lugha ya kwanza ya wanafunzi, ukosefu wa mazoezi ya kutosha, na mbinu zisizofaa za ufundishaji wa Kiswahili. Aidha, utafiti ulibaini kuwa baadhi ya walimu hawarekebishi makosa ya kimatamshi darasani, jambo ambalo huongeza changamoto ya kupata ufasaha katika lugha. Vilevile, mazingira ya kujifunzia na vitabu vinavyotumika havikidhi mahitaji ya kufundisha matamshi sahihi, jambo lililochangia makosa haya kuendelea kuwepo.Utafiti huu ulihitimisha kuwa kuwepo kwa mafunzo maalum ya matamshi, matumizi ya mbinu za kisasa kama vile teknolojia ya kurekodi na mazoezi ya pamoja yanayohusisha wanafunzi kwa njia ya maigizo na majadiliano, ni muhimu kwa kuboresha matamshi ya wanafunzi. Pia, walimu wanahimizwa kuzingatia kurekebisha makosa ya matamshi mara moja darasani kwa kuzingatia umuhimu wa ufasaha wa lugha katika mafanikio ya kitaaluma na mawasiliano ya kila siku.Kwa ujumla, utafiti huu unatoa mwanga muhimu juu ya changamoto za makosa ya kimatamshi katika elimu ya Kiswahili, na unaonyesha njia bora za kuboresha matokeo ya ufundishaji na kujifunza Kiswahili katika shule za upili za umma. Matokeo haya yanatoa msingi mzuri wa sera na mikakati ya kielimu itakayochangia kuimarisha matumizi ya lugha sanifu katika jamii.